Korali ya Mama Jusi Choir, inayohudumu katika Kanisa la Anglikana la Holy Trinity lililoko mjini Moshi, Tanzania, inajiandaa kwa sherehe kubwa ya kusherehekea miaka 50 ya huduma kwa Mungu kupitia nyimbo na mahubiri.
Sherehe hizi zitafanyika tarehe 28 Septemba 2025, kuanzia saa mbili asubuhi, katika kanisa la Holy Trinity Moshi ambako hii korali hufanyia ibada zake za kawaida.
Mama Jusi Choir ni miongoni mwa kwaya maarufu na zenye mvuto mkubwa katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwa imetoa mchango mkubwa katika kueneza Injili ya Yesu Kristo ndani ya Tanzania na hata nje ya mipaka yake. Kwa sasa, kwaya hii ipo tayari kumtukuza Mungu kwa yale aliyowawezesha kuyafanya kwa kipindi cha miaka 50.
Mama Jusi Choir ilianzishwa mwaka 1975, ikiwa na wanakwaya 11 pekee. Baada ya miaka 50, sasa ina wanakwaya zaidi ya 86, wakiwemo vijana kwa wazee, wote wakiwa na lengo moja kuu: kuimba na kumtangaza Mungu.
Katika kipindi chote cha huduma yao, wamefanikiwa kufanya huduma ya uinjilisti katika nchi mbalimbali zikiwemo Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Uganda na Rwanda, ambako wamehubiri kupitia nyimbo zao za Injili.
Katika siku yenyewe ya sherehe, kutakuwa na matukio mengi yatakayoashiria kuwa ni tukio la kipekee. Sherehe zitaanza kwa nyimbo za shukrani, ambapo walioalikwa watapata fursa ya kumshukuru Mungu kwa yale aliyoyafanya kupitia Mama Jusi Choir.
Baada ya hapo, kutaimbwa nyimbo mbalimbali kutoka kwa kwaya mbalimbali zilizoalikwa, zikiwemo Mama Jusi Choir wenyewe, Bethlehem Choir kutoka Moshi, na VCC Tanzania Choir. Pia kutakuwa na tukio la Harambee, kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia kwaya kununua vifaa vya muziki vya kisasa, vitakavyowawezesha kuendelea na huduma ya Mungu kwa njia ya kisasa.
Wageni mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe hizi ni pamoja na viongozi wa juu wa kanisa na taasisi za uinjilisti, wakiwemo Rev. Selestine Bulemo, atakayekuwa Mwenyekiti Mkuu; Mhe. Yonah Sonelo, atakayekuwa Mgeni Rasmi; na Mch. Daniel Mgogo, atakayehubiri Neno la Mungu siku hiyo.
Katika kuendeleza huduma ya Mungu kupitia muziki, kiongozi mkuu wa Mama Jusi Choir, Titus Ezra Sambay, amechukua hatua binafsi kwa kutoa wimbo mpya aliouachia rasmi tarehe 1 Julai 2025, uitwao "Mungu Unanipenda", akimaanisha “Mungu ananipenda”. Wimbo huu ameimba pamoja na Rose Muhando, mmoja wa waimbaji mashuhuri wa kimataifa wa nyimbo za injili.
Titus alieleza kuwa aliandika wimbo huu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake na nguvu alizomwonyesha katika safari yake ya muziki, akisema:
“Ni wimbo niliouandika kumshukuru Mungu kwa upendo wake na nguvu zake zilizoniongoza katika safari yangu ya muziki.”
Alibainisha kuwa huu si wimbo wa Mama Jusi Choir kama kikundi, bali ni wa kwake binafsi kama msanii, na sasa unapatikana kwenye YouTube channel yake binafsi iitwayo Titus Band, ambako watu duniani kote wanaweza kuusikiliza.
Miaka 50 ya huduma si jambo dogo. Mama Jusi Choir inawaalika kila mtu, iwe ni wanachama wa kwaya, washirika wa huduma, wapenzi wa muziki wa injili, au raia wa kawaida, kuhudhuria sherehe hii ya kumshukuru Mungu kwa mahali alipotutoa na alipotufikisha.
Wanaotaka kutoa michango ya kusaidia huduma ya kwaya hii wanaweza kutumia akaunti ya benki ya CRDB yenye namba 0152 3243 088 00, au kupitia simu ya MIXX BY YAS: 06789 967 79.
Titus Ezra, kama kiongozi mkuu wa kwaya, alisisitiza kuwa hii siyo sherehe ya kikundi pekee, bali ni wakati wa kukumbuka kwamba Mungu ndiye aliyewajenga, kuwalinda, na kuwabariki wanaohudumu kupitia talanta ya muziki.
Kwa maneno yake mwenyewe, alipoongea na Paradise alisema:
“Ninawaalika nyote katika sherehe ya miaka 50 yetu. Njooni tumshukuru Mungu, tukumbuke alikotutoa, tuazimie kuendelea na huduma yake kwa nguvu na neema zake.”
Sherehe ya miaka 50 ya Mama Jusi Choir ni tukio kubwa litakalomheshimu Mungu, kuimarisha mshikamano miongoni mwa wapenzi wa muziki wa Injili, na kusaidia kwaya kusonga mbele kwa hatua nyingine.
Rev. Selestine Bulemo, atakayekuwa Mwenyekiti Mkuu
Mhe. Yonah Sonelo, atakayekuwa Mgeni Rasmi
Mch. Daniel Mgogo, atakayehubiri Neno la Mungu siku hiyo
Titus Sambay na Rose Muhando
Wanamama wa Mama Jusi Choir watakuwa vinara wa kuongoza sifa na ibada kama wenyeji wa tukio
VCC Tanzania Choir nao wataimba katika tukio hili
Tazama wimbo wa Titus, Kiongozi Mkuu wa Mama Jusi Choir aliouimba na Rose Muhando kwenye YouTube